Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania

lbl_iso_certified

PROF. TEMU AZINDUA BARAZA LA WAFANYAKAZI LA MAMLAKA YA AFYA YA MIMEA NA VIUATILIFU TANZANIA (TPHPA)

Watumishi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) wametakiwa kutumia mikutano ya Baraza la wafanyakazi kujadili mambo yanayoleta tija kwa ajili ya kuimarisha utendaji wa kazi miongoni mwao ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea. Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TPHPA Prof. Andrew Temu alipokuwa akizungumza katika ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi la Kwanza la Mamlaka hiyo mapema leo Februari 27,2023 katika mkutano uliofanyika ndani ya ukumbi wa mikutano wa Mamlaka hiyo Arusha Ngaramtoni. Akizungumza katika mkutano huo Prof.Temu amesema ili kufikia malengo ya Mamlaka hiyo ambayo ni pamoja na kuifanya Tanzania kuongeza Kufanya biashara ya mimea na mazao hapa nchini na kimataifa ni muhimu kufanya kazi kwa ufanisi na kutumia vyema Baraza la wafanyakazi kwa kuzungumzia Mipango ya kusaidia Mamlaka hiyo. Amefahamisha kuwa TPHPA ni taasisi ya kisayansi, RAAWU ni chama cha wafanyakazi kwenye tasisi za elimu ya juu, sayansi, tekinolojia na ufundi stadi. Hivyo basi Baraza hilo la Wafanyakazi linatakiwa kuhakikisha linafahamu vyema undani wa jinsi sayansi ilivyo msingi wa utekelezaji wa majukumu yao. Pia amewataka kila mjumbe wa baraza kujiongeza kwa kujisomea, kuhudhuria semina za kisayansi na hata kujiandikisha kwenye kozi fupi, kutegemeana na taaluma na ngazi yake kwenye sehemu au kitengo. Menejimenti nayo ijitahidi kuandaa semina zinazowajengea ufahamu wajumbe wa baraza la wafanyakazi kuhusu sayansi na tekinolojia. Amesema ni vyema ushauri unaotolewa na baraza la wafanyakazi la TPHPA ukaheshimu sayansi, kazi za wanasayansi na majukumu ya wafanyakazi wezeshi katika taasisi ya kisayansi. "Kwa mfano – Ulimwenguni kote hofu kubwa iliyoko kwa wafanyakazi ni athari za Artificial Intelligence (Akili Bandia). Ni muhimu sana baraza la wafanyakazi likaelewa tekinolojia hii ya Akili Bandia na zinavyoathiri ajira. Ni muhimu baraza la wafanyakazi la taasisi kama TPHPA kuwa mstari wa mbele, sio katika kuizuia kwa sababu haizuiliki, bali kushauri na kupanga mikakati jinsi ambavyo tekinolojia itakuwa nyenzo ya wafanyakazi kutekeleza majukumu yao badala ya kuwa ni mbadala wa ajira zao" amesisitiza Prof. Temu Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA Prof. Joseph Ndunguru ametoa wito kwa wajumbe na washiriki wote wa Baraza hilo kutumia fursa hiyo waliyoipata ya kushiriki Baraza hilo kuhoji na kutoa mapendekezo chanya yatakayokuwa na msaada kwa mamlaka hiyo ili hatimaye mchango wa TPHPA uonekane katika jitihada za pamoja katika kuiletea nchi maendeleo.