MABILIONI YAWEKEZWA KUIMARISHA AFYA YA MIMEA, EU YAPONGEZA
June 10, 2026 Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Christine Grau, ametembelea Makao Makuu ya Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) jijini Arusha kushuhudia maendeleo yaliyofikiwa kupitia Mradi wa STREPHIT unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na kutekelezwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).
Ziara hiyo ilihusisha hafla ya kukata utepe kuashiria hatua zilizofikiwa katika ukarabati wa maabara za afya ya mimea nchini. Mara baada ya kuwasili, Mhe. Grau alipokelewa na Mwakilishi wa FAO nchini Tanzania, Nyabenyi Tito Tipo, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru, pamoja na viongozi na menejimenti ya TPHPA kabla ya kupata maelezo kuhusu utekelezaji wa mradi huo na mafanikio yaliyopatikana hadi sasa. Akimkaribisha mgeni huyo, Profesa Ndunguru alisema uwekezaji huo umefanyika katika kipindi muhimu ambapo dunia inakabiliwa na ongezeko la changamoto za wadudu na magonjwa ya mimea yanayovuka mipaka, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na mahitaji makubwa ya biashara salama ya mazao ya kilimo inayokidhi viwango vya kimataifa. Alitoa shukrani kwa Umoja wa Ulaya na FAO kwa ushirikiano unaoendelea kuimarisha sekta ya afya ya mimea nchini.
Aidha, Profesa Ndunguru alisema mpango huo unahusisha ukarabati wa maabara kuu nane pamoja na uanzishwaji wa maabara ndogo 20 katika vituo vya mipakani, hatua ambayo itaongeza uwezo wa Tanzania katika kugundua, kufuatilia na kudhibiti wadudu na magonjwa ya mimea, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza ushindani wa mazao ya Tanzania katika masoko ya kimataifa. Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Christine Grau alisema Umoja wa Ulaya unajivunia mafanikio yaliyofikiwa kupitia Mradi wa STREPHIT na kusisitiza kuwa afya bora ya mimea ni msingi muhimu wa usalama wa chakula, maendeleo ya kilimo na biashara endelevu. Alibainisha kuwa maboresho ya maabara na mifumo ya ufuatiliaji wa visumbufu vya mimea yataisaidia Tanzania kukabiliana kwa ufanisi zaidi na changamoto za afya ya mimea huku yakifungua fursa zaidi za masoko ya kimataifa kwa mazao ya kilimo.
Kwa mujibu wa viongozi wa mradi huo, uwekezaji huo pia unachangia juhudi za kikanda na kimataifa za kuimarisha usalama wa kibayolojia kwa kupunguza hatari ya kuenea kwa wadudu vamizi na magonjwa kupitia biashara ya kimataifa. Hafla ya kukata utepe imeelezwa kuwa ishara ya ushirikiano imara kati ya Serikali ya Tanzania, Umoja wa Ulaya, FAO na TPHPA katika kujenga mfumo wa kisasa na endelevu wa afya ya mimea kwa manufaa ya Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki