TPHPA Yafanikisha utoshelevu wa chakula Nchini
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Prof. Joseph C. Ndunguru, amesema mamlaka hiyo imefanikiwa kudhibiti kwa kiasi kikubwa visumbufu vya mazao nchini, hatua iliyosaidia kuokoa maelfu ya ekari na kuongeza uzalishaji wa chakula. Akizungumza na waandishi wa habari Machi 24, 2026 katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, alisema mafanikio hayo yanatokana na mikakati madhubuti ya kudhibiti wadudu na magonjwa ya mimea.
Prof. Ndunguru alibainisha kuwa katika kukabiliana na baa la panya, TPHPA ilitekeleza operesheni katika mikoa 19, wilaya 68, kata 638 na vijiji 1,669, ambapo wakulima 66,511 walifikiwa na huduma hiyo na kuokoa ekari 408,109 za mazao. Aidha, alisema zaidi ya ndege waharibifu aina ya kwelea kwelea milioni 231 walidhibitiwa katika halmashauri 23, hatua iliyosaidia kuokoa zaidi ya tani 1,611,000 za nafaka zikiwemo mpunga, uwele na mtama katika mikoa mbalimbali nchini.
Ameeleza kuwa udhibiti huo ulifanyika kwa kutumia mbinu za anga na ardhini, ikiwemo kunyunyizia viuatilifu kwa ndege, ndege nyuki na vinyunyizi vya kubebwa mgongoni, kwa kushirikiana na Shirika la Kudhibiti Nzige wa Jangwani (DLCO-EA). Mbali na hilo, mamlaka ilidhibiti viwavijeshi katika hekta 219,411 kwenye wilaya 49 na kuokoa zaidi ya tani 529,347 za mazao ya nafaka, pamoja na kudhibiti nzige ikiwemo nzige wekundu katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Katika hatua nyingine, Prof. Ndunguru alisema TPHPA imeendelea kuimarisha tafiti na ushirikiano wa kikanda kwa kuchunguza magonjwa ya mazao kwa teknolojia ya kisasa ya DNA, pamoja na kuwezesha mikataba ya biashara ya mazao kati ya Tanzania na Malawi. Amesema hatua hizo zinalenga kuongeza masoko ya mazao, kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi, na kuimarisha usalama wa chakula nchini.