Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania

lbl_iso_certified

TPHPA  YAWEKA MIKAKATI YA KUZALISHA MAZAO YASIYO NA SUMU KULINDA AFYA ZA WALAJI

Imewekwa: 25 Jun, 2024
TPHPA  YAWEKA MIKAKATI YA KUZALISHA MAZAO YASIYO NA SUMU KULINDA AFYA ZA WALAJI

 

Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania TPHPA imefanikiwa kuweka mikakati ya msingi inayolenga kuzalishwa mazao yasiyo na masalia ya Viuatilifu ili kupanua wigo katika soko la dunia kwa mustakabali wa kulinda afya za Binadamu na Mazingira.

Akizungumza katika Mkutano wa Mwaka wa kwanza wa Wadau wa Afya ya Mimea na Viuatilifu Uliofanyika Juni 21. 2024 katika Ukumbi wa Makao Makuu ya Mamlaka hiyo Ngaramtoni, Jijini Arusha. Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Kaganda akimwakilisha Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe aliyetarajiwa kuwa Mgeni Rasmi, ameipongeza Mamlaka hiyo kwa jitihada zake kubwa za kuleta mabadiliko na uzalishaji wenye tija katika Sekta ya Kilimo.

Aidha ameongeza kuwa, Sekta ya Kilimo ni mkombozi kwani inategemewa kuongeza ajira za vijana na wanawake, kutoa ajira za stara, kuimarisha mfumo wa chakula na kuongeza pato la taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

"Serikali kwa kutambua umuhimu wa sekta hii muhimu imeongeza bajeti kutoka bilioni 970 kwa mwaka wa fedha 2023-2024 kufikia tilioni 1.2 kwa mwaka wa fedha 2024-2025, hii yote ni kuhakikisha tunajiimarisha katika soko la dunia na kuzidi kuwa bora katika uzalishaji wa chakula cha kutosha" amesema,

"Nawasisitiza Mamlaka ya TPHPA kuhifadhi mbegu za asili, hii itasaidia kuepuka upotevu wa mbegu bora zinazotegemewa katika ushindani wa soko la dunia" amesisitiza Kaganda.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPHPA Prof. Andrew Temu amesema kuna muelekeo wa mamlaka hiyo kutimiza malengo yake ya kuboresha afya za watu kutokana na juhudi na mikakati mbambali inayowekwa.

Ameongeza kwamba, TPHPA inatambua juhudi za serikali katika utekelezaji wa majukumu yao, ushauri na maelekezo muhimu yenye lengo la kuhakikisha mamlaka hiyo inaimarika na kuendelea kufanya vizuri.

"Tunaendelea na jitihada za kutanua wigo wa kilimo cha umwagiliaji lakini pia kupambana na changamoto mbalimbali zikiwemo usugu wa viuatilifu, kupotea kwa vinasaba katika mimea ya asili, ubunifu na mbinu juu ya viuatilifu sambamba na hayo tunajipanga kwa matumizi ya akili mnemba ili kuendana na Maendeleo ya Teknolojia lakini pia kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi" ameeleza Prof. Temu.