Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania

lbl_iso_certified

TPHPA yapokea ugeni wa Wizara ya Fedha kutathimini utekelezaji wa mradi wa kuimarisha huduma za afya ya mimea na usalama wa chakula

Imewekwa: 11 Mar, 2026
TPHPA yapokea ugeni wa Wizara ya Fedha kutathimini utekelezaji wa mradi wa kuimarisha huduma za afya ya mimea na usalama wa chakula

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Udhibiti wa Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Prof. Joseph Ndunguru, amepokea ugeni wa timu maalumu kutoka Wizara ya Fedha Tanzania waliotembelea makao makuu ya taasisi hiyo kwa lengo la kupitia na kujionea utekelezaji wa mradi wa kuimarisha huduma za afya ya mimea na usalama wa chakula nchini.

Timu hiyo ya Wizara ya Fedha ilifika katika ofisi za TPHPA  Machi 111, 2026 kwa ajili ya kufanya tathmini ya maendeleo ya mradi unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikal, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Umoja wa Ulaya (EU), unaolenga kuboresha sekta ya mimea, kuongeza usalama wa chakula na kuimarisha uwezo wa wakaguzi wa afya ya mimea nchini.

Akizungumza wakati wa mapokezi ya ugeni huo, Prof. Ndunguru alieleza kuwa mradi huo una mchango mkubwa katika kuboresha miundombinu na mifumo ya ukaguzi wa afya ya mimea, jambo litakalosaidia kupunguza changamoto zinazowakumba wakulima na wafanyabiashara wa mazao ya kilimo hasa katika masoko ya kimataifa.

Alisema kupitia mradi huo, vituo vya ukaguzi mipakani vinaendelea kuboreshwa, maabara za kisasa zinakarabatiwa na kununuliwa vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa magonjwa na wadudu waharibifu wa mazao. Aidha, mfumo wa kidigitali wa ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu mashambani unaendelea kuanzishwa ili kurahisisha ufuatiliaji wa afya ya mimea.

Kwa upande wao, wajumbe wa timu kutoka Wizara ya Fedha walipata fursa ya kutembelea baadhi ya vitengo vya TPHPA na kuona utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazofadhiliwa na mradi huo, ikiwa ni pamoja na maandalizi ya matumizi ya teknolojia ya ndege zisizo na rubani (drones) katika utafiti na uchunguzi wa visumbufu vya mazao.

Mradi huo wa miaka mitatu unaotekelezwa na FAO kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya unatarajiwa kutumia zaidi ya dola milioni 9 za Marekani, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 22 za Kitanzania, kwa lengo la kuimarisha afya ya mimea na kuongeza ushindani wa mazao ya Tanzania katika soko la kimataifa.