Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania

lbl_iso_certified

NAIBU WAZIRI MHE. SILINDE AIAGIZA TPHPA KUJENGA MAABARA ZA KISASA KATIKA VITUO VYA UKAGUZI RUSUMO NA MUTUKULA

Imewekwa: 26 Jan, 2025
NAIBU WAZIRI MHE. SILINDE AIAGIZA TPHPA KUJENGA MAABARA ZA KISASA KATIKA VITUO VYA UKAGUZI RUSUMO NA MUTUKULA

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb), ameielezeka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kujenga Maabara za Kisasa katika vituo vya ukaguzi vilivyopo katika mipaka ya Rusumo (Ngara) na Mutukula, ili kuboresha utendaji kazi wa vituo hivyo na kuharakisha mchakato wa ukaguzi wa mazao.

Mhe. Silinde alitoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya katika vituo hivyo vilivyopo mkoani Kagera tarehe 23 Januari 2025. Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kukagua utendaji kazi wa vituo hivyo, kubaini changamoto zinazojitokeza na kuzitolea ufumbuzi ili kuongeza ufanisi wa shughuli zinazofanyika katika mipaka hiyo ya biashara.

Akizungumza na viongozi wa TPHPA, Naibu Waziri Silinde alieleza kuwa, ujenzi wa maabara za kisasa katika vituo vya Rusumo na Mutukula utahakikisha kuwa huduma za ukaguzi na utoaji wa vyeti vya usafi wa mazao zinafanyika kwa haraka na kwa ubora wa hali ya juu, huku akisisitiza umuhimu wa maabara hizo katika kuhakikisha usalama wa mazao yanayokwenda nje ya nchi na yanayoingizwa nchini.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph Nduguru, alithibitisha kuwa agizo la Naibu Waziri linatekelezwa na kusema kuwa mipango ya ujenzi wa maabara hizo itazingatia viwango vya kisasa na itatekelezwa kwa ufanisi. Alisema kuwa hatua hii ni muhimu katika kuboresha huduma za ukaguzi na kuongeza ufanisi katika biashara ya kimataifa ya mazao.

 

Aidha, Kaimu Meneja wa TPHPA Kanda ya Ziwa, Bi. Mary Leina, alieleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024, vituo vya Rusumo na Mutukula vilifanya kazi nzuri kwa kukagua mazao yenye uzito wa tani 331,537. TPHPA ilikusanya zaidi ya shilingi 374 milioni kutokana na huduma za ukaguzi, na sehemu kubwa ya mazao hayo ilisafirishwa kwenda nchi za nje, hasa mchele, mtama, maharage, na molasses.

 

Bi. Leina aliongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025, Mpaka wa Rusumo tayari umehakiki tani 98,275.67 za mazao, na kuingiza fedha zaidi ya shilingi milioni 140,000,000, huku Mpaka wa Mutukula ukikagua tani 51,692.003 za mazao na kupata kiasi cha shilingi milioni 101,718,772.

 

"Mpaka wa Rusumo na Mutukula ni muhimu sana katika biashara ya mazao ya kilimo, na kupitia ujenzi wa maabara za kisasa, tunaamini tutaongeza tija na kuhakikisha kuwa mazao yanayohitaji kusafirishwa nje ya nchi yanakaguliwa kwa ufanisi zaidi," alisema Bi. Leina.

 

Hii ni hatua kubwa kwa Tanzania, kwani inaonesha dhamira ya serikali kuboresha mifumo ya ukaguzi wa mazao na kuhimiza biashara ya kimataifa, sambamba na kuhakikisha usalama wa afya ya mimea na viuatilifu katika biashara ya kimataifa.