BW. MWELI AMEIPONGEZA MAMLAKA KWA JUHUDI ZAKE ZA KUFANIKISHA UFUNGUZI NA KUYALINDA MASOKO YA MAZAO YA KILIMO NDANI NA NJE YA NCHI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, amefanya ziara ya kimkakati katika ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) yaliyopo Ngaramtoni, Arusha, tarehe 21 Agosti 2025. Katika ziara hiyo, Bw. Mweli ameipongeza Mamlaka kwa juhudi zake za kufanikisha ufunguzi na kuyalinda masoko ya mazao ya kilimo nje ya nchi pamoja na kusimamia kwa weledi ukaguzi wa mazao.
Aidha, Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa kuwa na taarifa za mara kwa mara kuhusu mwenendo wa biashara ya mazao. Ameielekeza mamlaka kuhakikisha kuwa inawasilisha ripoti za kila wiki kwa Wizara ya Kilimo zikihusu mwenendo wa usafirishaji wa mazao nje ya nchi. Hatua hii inalenga kuwapa uelewa watoa maamuzi ili kuzijua changamoto za biashara ya kilimo na kuweka mikakati ya kuzitatua, sambamba na kuwasaidia wakulima kujua masoko yanataka nini na mazao gani kwa sasa yanahitajika katika nchi mbalimbali.
Pamoja na hayo, Bw. Mweli amepongeza uboreshwaji wa vifaa vya maabara vya TPHPA, ikiwemo mashine za kisasa za uchambuzi wa viuatilifu na mabaki ya viuatilifu kwenye mazao yanayosafirishwa nje ya nchi. Amesema hatua hiyo inaongeza imani kwa masoko ya kimataifa na inalinda afya ya walaji wa ndani kupitia mazao salama na yenye ubora.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph Ndunguru, amesema ujio wa Katibu Mkuu ambaye pia ni mtunga sera ni hatua muhimu inayokwenda kuinua shughuli na majukumu yanayotekelezwa na Mamlaka. Amesisitiza kuwa ziara hiyo imeongeza hamasa Kwa Mamlaka katika kuhakikisha sekta ya kilimo nchini inakua kwa ushindani wa kimataifa.