Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania

lbl_iso_certified

TPHPA yaja na Teknolojia Mpya Kukabili Magonjwa na wadudu waharibifu wa mazao wilayani Kilolo Mkoani Iringa

Imewekwa: 12 Oct, 2025
TPHPA yaja na Teknolojia Mpya Kukabili Magonjwa na wadudu waharibifu wa mazao wilayani  Kilolo Mkoani Iringa

Wakulima wa mazao ya mboga mboga na matunda wilayani Kilolo mkoani Iringa wameeleza kuwa changamoto za magonjwa na wadudu waharibifu zimekuwa kikwazo kikubwa katika uzalishaji, hali inayosababisha hasara na kushusha tija ya kilimo.

Wakizungumza na katika vijiji vya Ruaha Mbuyuni, Mtandika na Msosa, wakulima Bi Salome Isack na Bwana Husein Kiwela walisema magonjwa kama mnyauko wa vitunguu yameathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji wao, huku baadhi ya wakulima wakilazimika kuacha kulima zao hilo kutokana na gharama kubwa za kudhibiti visumbufu.

“Tunatumia fedha nyingi kununua viuatilifu lakini matokeo yake hayaridhishi. Wadudu na magonjwa yanarudi mara kwa mara,” alisema Bi Isack.

Kufuatia changamoto hizo, Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imeanza kutumia teknolojia mpya ya Portable DNA Sequencing ili kubaini visababishi vya magonjwa na visumbufu vya mimea moja kwa moja shambani.

Mtaalamu wa teknolojia hiyo kutoka TPHPA, Bwana Rosca Willium, alisema kupitia kifaa hicho wamebaini changamoto kadhaa zinazokabili wakulima hao, na kwamba wataendelea kutoa elimu kwa wakulima ili kuhakikisha wanatumia mbinu sahihi za kudhibiti magonjwa kwa njia endelevu.

“Tumeweza kuona kwa haraka aina za visumbufu vinavyoshambulia mazao. Tunatarajia kutoa mafunzo zaidi ili wakulima waweze kudhibiti kwa ufanisi,” alisema Willium.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru, alisema teknolojia hiyo inalenga kuongeza kasi ya upatikanaji wa majibu ya kitaalamu bila kusafirisha sampuli hadi maabara kuu, jambo litakalowasaidia wakulima kupata tiba sahihi kwa wakati.

“Tunataka suluhisho la magonjwa na wadudu lipatikane shambani shambani, kijiji kwa kijiji, kupitia matumizi ya teknolojia hii ya kisasa,” alisema Prof. Ndunguru.

Wakulima wa Kilolo wamepongeza hatua hiyo ya TPHPA na kueleza kuwa inawapa matumaini mapya ya kufufua uzalishaji wa mazao ya mboga mboga na matunda kwa tija zaidi.