Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania

lbl_iso_certified

TPHPA YAFUNGUA FURSA KWA WAKULIMA KUPITIA UDHIBITI WA VISUMBUFU NA UFUNGUZI WA MASOKO YA KIMATAIFA YA MAZAO

Imewekwa: 27 Aug, 2026
TPHPA YAFUNGUA FURSA KWA WAKULIMA KUPITIA UDHIBITI WA VISUMBUFU NA UFUNGUZI WA MASOKO YA KIMATAIFA YA MAZAO

Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imeendelea kuweka mazingira yanayowawezesha wakulima kuongeza uzalishaji na kipato kupitia udhibiti wa visumbufu na magonjwa ya mimea. Kwa kudhibiti kwelea kwelea, viwavi jeshi na baa la panya, Mamlaka imepunguza uwezekano wa wakulima kupoteza mazao, hivyo kutoa fursa ya kuongeza tija na kipato kutokana na mavuno yaliyookolewa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, leo Agosti 27, 2026, katika Ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph Ndunguru, amesema hatua mbalimbali zinazotekelezwa na Mamlaka katika kudhibiti visumbufu zimekuwa na mchango mkubwa katika kulinda uzalishaji wa wakulima na kupunguza hasara zinazoweza kusababishwa na milipuko ya visumbufu na magonjwa ya mimea.

Prof. Ndunguru amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, TPHPA ilidhibiti kwelea kwelea milioni 233.5 waliovamia wilaya 21, hatua iliyosaidia kuokoa takribani tani 1,092,780 za mazao ya nafaka, zikiwemo mtama, uwele na mpunga. Aidha, udhibiti wa viwavi jeshi katika Halmashauri 52 uliwezesha kuokoa takribani tani 342,787.5 za mazao ya nafaka ambazo zingeweza kuharibiwa na visumbufu hivyo.

Amesema mafanikio hayo yanafungua fursa kwa wakulima kuongeza tija na kipato kwa kuwa mazao yaliyookolewa yanaendelea kuwa sehemu muhimu ya uzalishaji na biashara. Sambamba na hilo, TPHPA imeendelea kutumia teknolojia za kisasa, ikiwemo PCR na DNA Sequencing, katika kutambua kwa usahihi visumbufu na magonjwa ya mimea, hatua inayowezesha wataalamu kutoa ushauri na kuchukua hatua stahiki za udhibiti.

Kwa upande mwingine, Prof. Ndunguru amesema TPHPA imeendelea kufungua fursa za masoko ya kimataifa kwa mazao ya Tanzania, ikiwemo parachichi kwenda China, India na Afrika Kusini, mahindi ya njano kwenda Misri, pamoja na mazao mbalimbali kwenda Seychelles. Hatua hiyo inatoa fursa kwa wakulima kujikita zaidi katika kilimo-biashara, kuongeza uzalishaji wa mazao yenye ubora na kupata masoko yenye thamani kubwa, huku TPHPA ikiendelea kuhakikisha mazao yanakidhi matakwa ya afya ya mimea ya nchi wanunuzi.