Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania

lbl_iso_certified

MCHECHU AIPONGEZA MAMLAKA YA AFYA YA MIMEA NA VIUATILIFU TANZANIA (TPHPA) KWA ONGEZEKO LA MADUHULI YA SERIKALI.

Imewekwa: 21 Feb, 2024
MCHECHU AIPONGEZA MAMLAKA YA AFYA YA MIMEA NA VIUATILIFU TANZANIA (TPHPA) KWA ONGEZEKO LA MADUHULI YA SERIKALI.

Msajili Hazina Ndugu Nehemiah Mchechu, leo tarehe 20 Februari, 2024 ametembelea Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) iliyopo jijini Arusha, Tanzania. Katika  ziara hii, Bw. Mchechu alipokelewa na kufanya mazungumzo na Prof. Joseph Ndunguru, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo. Katika mazungumzo yao, Prof. Ndunguru amemueleza Msajili wa Hazina kuhusu mikakati ya mamlaka katika kuboresha utendaji wa mamlaka na ukusanyaji wa maduhuli kwa niaba ya Serikali . Kwa upande wake, Bw. Mchechu amempongeza Prof. Ndunguru pamoja na menejimenti ya mamlaka kwa utendaji wenye tija na kimkakati  katika kusimamia viuatilifu ikiwa ni sehemu ya kusaidia wakulima na kuhakikisha uwepo wa usalama wa chakula Tanzania.

 

Aidha, Msajili ameonesha kuridhishwa kwake na utendaji wa shirika kuendana na maelekezo aliyoyatoa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuwa akiongea na watendaji wakuu kwenye Kikao kilichofanyika Agosti, 2023. Rais Samia kupitia maono yake ya 4R ameendelea kusisitiza ufanisi na utendaji bora wa mashirika ya umma ili kuhakikisha yanakuwa na manufaa kwa Watanzania kama malengo ya kuanzishwa mashirika hayo yalivyoainishwa.

 

Ziara hii ni muendelezo wa mapinduzi ya utendaji  wa masharika ya umma yanayosimamiwa na Msajili wa Hazina. Ni rai ya Msajili wa Hazina kwa mashirika yote kujitathmini na kuona namna ambayo wataweza kuleta tija na kuongeza makusanyo kwa nia ya kukuza uchumi wa Tanzania. Msajili amemuhakikishia Prof. Nduguru ushirikiano wake na ofisi yote ya Msajili wa Hazina katika kuhakikisha Mamlaka inaongeza ufanisi na inakuwa taasisi ya mfano katika kutoa huduma na kuongeza ufanisi.

 

Mwisho, Msajili Mchechu alitumia nafasi hii kuwaeleza menejimenti  ya mamlaka kuhusu mabadiliko yanayoendelea katika ofisi ya Msajili wa Hazina na muendelezo wa uanzishwaji wa Mamlaka mpya ya Uwekezaji wa Umma.