TPHPA YAWAJENGEA UWEZO WAKAGUZI KUBORESHA HUDUMA KWA WAFANYABIASHARA NA WADAU
Morogoro, Novemba 16, 2026. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Ndugu Oshingi Shilla, amefungua mafunzo ya siku kumi kuhusu afya ya mimea na ukaguzi wa viuatilifu yanayofanyika katika Ukumbi wa Maji House, mkoani Morogoro, kuanzia Novemba 16 hadi 25, 2026. Mafunzo hayo yanawakutanisha wakaguzi kutoka vituo mbalimbali vya ukaguzi vya TPHPA nchini kote kwa lengo la kuwaongezea ujuzi na uwezo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Ndugu Shilla amesema mafunzo hayo yatasaidia kurahisisha utoaji wa huduma kwa wadau na kupunguza changamoto zinazojitokeza katika vituo vya ukaguzi. Amesema uwepo wa wakaguzi wenye ujuzi na maarifa ya kutosha utawanufaisha wafanyabiashara na wadau kupitia upatikanaji wa huduma bora, zenye ufanisi na zinazotolewa kwa wakati. Aidha, amewataka washiriki kuzingatia maadili ya kazi na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na weledi.
Kwa upande wake, Meneja wa Sehemu ya Usimamizi wa Usafi wa Mimea na Karantini ya Taifa, Bw. Musa Paul Chidinda, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwaongezea wakaguzi maarifa na ujuzi katika usimamizi wa afya ya mimea na ukaguzi wa viuatilifu ili kuimarisha utekelezaji wa majukumu yao katika vituo vyote nchini.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa na manufaa kwa wafanyabiashara na wadau wa sekta ya mimea nchini, ambao wataendelea kunufaika na uwepo wa wakaguzi wenye mafunzo na uelewa wa kutosha katika vituo vya ukaguzi. Hali hiyo itasaidia kurahisisha michakato ya ukaguzi, kupunguza changamoto za utoaji huduma na kuweka mazingira rafiki ya biashara, huku ikichangia ulinzi wa afya ya mimea na kukuza biashara ya mazao ya kilimo ndani na nje ya nchi.