TPHPA YAADHIMISHA SIKU YA KIMATAIFA YA AFYA YA MIMEA KATIKA VIWANJA VYA AZIMIO LA ARUSHA MEI 12, 2025

Arusha, 12 Mei 2025– Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Afya ya Mimea yamefanyika katika viwanja vya Azimio la Arusha, yakiwa ni ya pili tangu kuanzishwa kwake mwaka 2024. Kaulimbiu ya mwaka huu ilikuwa “Umuhimu wa Afya ya Mimea katika Afya Moja,” ikilenga kuelimisha umma kuhusu mchango wa afya ya mimea katika maisha ya binadamu, ustawi wa wanyama na mazingira.
Akizungumza katika maadhimisho hayo kama mgeni rasmi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Umwagiliaji na Ushirika, Dkt. Stephen Nindi, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia dhana ya “Afya Moja” inayounganisha sekta za afya ya binadamu, wanyama na mimea kwa lengo la kufanikisha ustawi wa pamoja.
“Afya ya mimea ni msingi wa uzalishaji wa chakula na afya ya binadamu. Hatutakuwa salama endapo tutapuuza kipengele chochote cha mfumo wa ikolojia,” alisema Dkt. Nindi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Prof. Joseph Ndunguru, alieleza kuwa Tanzania kupitia TPHPA imefanikiwa kuongeza usalama wa chakula, kuimarisha tija katika kilimo na kufungua masoko ya kimataifa kwa mazao ya kilimo.
Miongoni mwa mafanikio yaliyotajwa na Prof. Ndunguru ni pamoja na udhibiti wa visumbufu vya mimea kama panya, nzige, kwelea kwelea na viwavi jeshi. Alisema TPHPA imesimamia usafirishaji wa tani milioni 5.5 za mazao ya kilimo zenye thamani ya shilingi trilioni 15.6.
Aidha, alieleza kuwa mamlaka hiyo imefanikiwa kufungua masoko ya kimataifa kwa mazao kama parachichi, vanilla, kahawa, tumbaku na karafuu. Vilevile, miundombinu ya maabara imeboreshwa, ikijumuisha vifaa vya kisasa kama ndege za kunyunyizia viuatilifu, pamoja na uwekezaji katika ufuatiliaji wa afya ya mimea na hifadhi ya zaidi ya aina 10,000 za nasaba za mimea.
Katika hotuba yake ya kuhitimisha, Prof. Ndunguru alitoa pongezi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake katika kuboresha sekta ya kilimo, pamoja na Wizara ya Kilimo, viongozi wa mkoa wa Arusha na wadau wengine walioshiriki katika maandalizi na ufanikishaji wa maadhimisho hayo.
“Afya ya mimea ni msingi wa maisha. Tunapaswa kushirikiana kuihifadhi kwa ajili ya mustakabali wa taifa,” alisema Prof. Ndunguru.
Maadhimisho hayo yalijumuisha maonesho ya teknolojia za kilimo, warsha za kitaalamu, na mijadala kuhusu usalama wa chakula, matumizi sahihi ya viuatilifu, na umuhimu wa udhibiti wa visumbufu kwa wakati.